quote:
Originally posted by kariuki wa kihia**:
Ahsanta sikuwa najua kuwa neno chai lina uhusiano na bara hindi.
Mwalimu wetu wa somo la kiswahili aliniambia kuwa hii lugha ilitokana ama ilianzishwa na wa arabu na watu wa pwani ili waweze kuelewana lakini nauliza je,kwani Nchi ya Tanzania(ambayo wengi waijua kama 'the swahili country'ilikuwa imejaa waarabu kote? Samahani sikulisoma somo la historia katika shule ya Upili.
Wa Kihia,
Nimenena mara kwa mara. Kiswahili ni Kibantu, si Kiarabu hata chembe. Ndiyo, Kiswahili kimeazima asilimia fulani ya maneno kutoka kwa Kiarabu, lakini ukweli ni kwamba Kiswahili ni lugha ya Kibantu.
Waarabu walipotembelea pwani yetu, walieneza ustaarabu wao na hapo msamiati na istilahi nyingine zikapata mwanya wa kujipenyeza. Kwa bahati mbaya, Wazungu wa kwanza walipofika Afrika, walidhani Kiswahili ni lahaja moja ya Kiarabu. Ndiposa wakazua nadharia hii ya mseto wa Kiarabu na Kibantu.
Pia ni vizuri tukubaliane kwamba Kiswahili si Lugha ya Tanzania. Kusema ukweli, Kiswahili kilizuka Kenya, hasa Sehemu za kaskazini (Siu, Pate, Lamu) na utafiti uliofanywa umethibitsha jambo hili.
Kuna mambo manne yaliyochangia Kiswahili kionekane kama Lugha ya Tanzania
1. Jambo la kwanza ni misingi ya Kiisimu. Katika nchi ya Tanzania, asilimia kubwa ya lugha zina asili ya Kibantu. Kwa vile Kiswahili ni mojawapo ya lugha za Kibantu, uwiano huu ulifaa kusambaza na kufahamika kwa Kiswahili kuliko hali ilivyo nchini Kenya, ambako kuna mchanganyiko wa vikundi tofauti vya Kiisimu.
2. Jambo la Pili ni Historia. Kabla ya kuja kwa wabeberu, kulikuwa na biashara iliyokuwa ikiendelea barani kutoka Pwani. Misafara ya Bishara ilitoka Unguja, kupitia sehemu kadhaa nchini Tanzania, hadi mashariki mwa Kongo. Biashara hii ilisambaza Kiswahili barani Tanzania, lakini haikuwa maarufu nchini Kenya, ndiposa Kiswahili hakikusambaa sana. Wakoloni walipokuja, tayari Kiswahili kilikuwa kimejikita nchini Tanzania.
3. Jambo la tati ni kwamba wakati wa kusanifisha Kiswahili, lahaja ya Kiunguja ilichaguliwa. Waliochagua lahaja hii hawakuwa Waswahili, lakini wageni ambao walikuwa na malengo yao wenyewe. Ikilinganishwa na lahaja ya Kimvita, lahaja ya Kiunguja ilikuwa finyu mno na ilijaa Uarabu mwingi. Kama unavyokumbika, Unguja yalikuwa makao makuu ya milki za Omani. Wageni walituchagulia, walitutafunia, nasi hatukuwa na budi, ila kumeza.
4. Jambo la nne ni mfululuizo wa mambo yaliyotendeka wakati wa enzi ya kupata Uhuru. Mwalimu Nyerere alitia juhudi kuimarisha Kiswahili Tanzania ili kiende sambamba na sera yake ya Ujamaa. Kiswahili kilitumiwa kama chombo cha kipingana na udhalimu na ukoloni mamboleo. Wakati huo, sisi Wakenya tuling'ang'ania Kiingereza. Tuliuza urithi wetu kwa sahani moja ya Githeri kama Esau alivyouza urithi wake kwa kaka yake Yakubu.
Emotions are the greatest enemy of rational arguments